Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema, Serikali imedhamiria kuwainua Wasanii nchini kwa kuangalia upya sheria kandamizi zinazowabana kuuza kazi zao mtandaoni ili waweze kunufaika na kazi hizo.

Amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Tuzo za Bodi ya Filamu 2021, Waziri Bashungwa amesema Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Wasanii nchini, na hivyo ikaona umuhimu wa kuanzisha tuzo hizo kama sehemu ya kutambua mchango wa sanaa katika pato la Taifa.

Amesema kuondolewa kwa sheria kandamizi kutawawezesha Wasanii kuuza kazi zao mtandaoni, lakini pia Serikali itaweza kupata mapato yake stahiki bila usumbufu.

“Tunataka Vijana wetu wanaofanya sanaa waweze kujiajiri kupitia mitandao bila usumbufu wowote.” amesema Waziri Bashungwa

Waziri Bashungwa amesema jitihada za Serikali kuangalia namna ya kurekebisha mfumo utakaowezesha Wasanii kupata chochote kwa asilimia 50 kupitia nyimbo zao zinazopigwa radioni zinaendelea.

Naye, katibu wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kyago Kilonzo amesema, tuzo hizo ni kilio cha muda mrefu cha Wasanii ambacho Serikali imekisikia, na kuanzisha rasmi mwaka huu.

Amesema lengo la kuandaa tuzo hizo ni kuhamasisha Wawekezaji kwenye tasnia ya filamu, na kuhamasisha wadau kufanya kazi zenye ubora.

Vipengele vilivyoshindaniwa ni pamoja na tamthilia bora ya mwaka, filamu bora, mwigizaji bora wa kiume na wa kike wa mwaka, huku kaulimbiu ya tuzo hizo ikiwa ni Filamu ni Biashara.

Rais Samia kupokea taarifa ya Soko la Kariakoo
Msigwa: Zaidi ya watanzania 345,000 wamepata chanjo