Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amemtaka Kamishna Mkuu mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA, Dkt. Edwin Mheda kwenda kufanyakazi kwa bidii na ushirikiano wa hali ya juu kwa wafanyakazi wenzie atakao wakuta.
Ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es salaam mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kuapishwa kwa viongozi hao, ambapo amesema yuko tayari kushirikiana naye katika hali yeyote ile atakayokumbana nayo.
Dkt. Mpango amesema kuwa Dkt. Edwin ana kazi kubwa ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ili kuweza kuondokana na wastani wa shilingi Trilioni 1 na bilioni mia tatu ambapo ni kwa muda mrefu sasa pato hilo limeganda bila kuongezeka, huku mahitaji ya taifa yakiwa ni makubwa.
Aidha, Dkt. Mpango ametaja changamoto nyingine atakayo kumbana nayo kuwa ni sura ya mamlaka ya mapato Tanzania kuwa ina sura ya matope, akimaanisha kuwa haina uhusiano mzuri na wafanyabiashara pamoja na walipa kodi kwa ujumla, hivyo anao wajibu wa kwenda kushirikiana na watumishi wenzie atakao wakuta ili kuweza kuisafisha na kutengeneza mahusiano mazuri na walipa kodi.
”Dkt. Edwin Mhede karibu sana mamlaka ya mapato Tanzania, lakini kuna changamoto kubwa sana pale ambazo moja kwa moja unatakiwa kukabiliana nazo, nazo ni kuongeza kipato na kutengeneza mahusiano mazuri na wafanyabiashara pamoja na walipa kodi kwa ujumla,”amesema Dkt. Mpango
Hata hivyo, Dkt. Mpango ameongeza yeye na wizara yake wako tayari muda wowote kushirikana naye atakapo hitaji msaada au ushauri kuhusu masuala ya kazi.