Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amezindua magari ya kliniki tembezi ya kisasa nne, pikipiki 160, mashine 50 za ‘GeneXpert’ pamoja na mashine 179 za ECG zilizogharimu billioni 6.2 ambazo zitasaidia kupunguza idadi au kuondoa kabisa wagonjwa wasiofikiwa wanaougulia majumbani hapa nchini.
Dkt. Gwajima Amezindua Kliniki hizo leo Septemba 6, 2021 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, huku lengo likiwa ni kuboresha huduma za matibabu ya ugonjwa wa TB na Ukoma ili kuutokomeza nchini.
“Jumla ya Bilioni 6.2 zimetumika kununua magari haya ya kliniki tembezi na vifaa vya kutolea huduma za afya. Kiasi hiki ni kikubwa, sina budi kuwapongeza watumishi wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma kwa kufanikisha zoezi hili,” Amesema Dkt. Gwajima.
Amesema kuwa, Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2020, Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa takribani 135,000, huku kati ya hao waliofanikiwa kubainiwa na kuwekwa kwenye matibabu walikuwa 85,597 sawa na asilimia 63, na kusisitiza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye tatizo kubwa la Kifua Kikuu.
Aidha takribani watu 26,800 wamefariki katika kipindi cha mwaka 2020 licha yajitihada zinazofanywa na Wizara katika kufikia malengo ya kutokomeza Kifua Kikuu nchini.
Hata hivyo bado nguvu ya ziada inahitajika ili kuweza kuwafikia na kuwaibua wagonjwa takribani 49,403 ambao hawakuweza kuwaibaini na bado wanaendelea kuambukiza ugonjwa huo katika jamii yetu.
Dkt. Gwajima amebainisha kwamba Dhima ya Wizara yake ni kutokomeza kifua kikuu nchini kwa makundi maalum yanayotambulika katika ngazi ya jamii kwa ajili ya ushirikishwaji katika mapambano hayo.