Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa maelekezo matatu kwa Serikali kuhusu ununuzi wa mahindi ya wakulima, vituo vya kununulia mahindi pamoja na bei ya mbolea nchini.

Maelekezo hayo yametolewa leo tarehe 06 Septemba, 2021 na Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Daniel Chongolo Makao Makuu ya Chama Dodoma.

Katibu Mkuu ametoa maelekezo hayo, baada ya Chama kusikia malalamiko ya wakulima kuhusu uhaba wa masoko ya mahindi, ambapo Chama kimeilekeza Serikali kutafuta fedha kwa ajili ya kununua mahindi katika mikoa yenye uzalishaji mkubwa.

“Baada ya maagizo ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa katika ziara ya mwezi Julai mwaka huu kwenye mikoa ya Rukwa, Songwe na Mbeya, kuhusu utafutaji wa masoko ya mahindi, NFRA na Bodi ya Mazao Mchanganyiko ilitenga fedha kununua mahindi, na taarifa zilizopo ununuzi unasua sua kutokakana na fedha kuisha, sasa hatuwezi kukaa namna hii wakulima wetu hawana pa kuuza mahindi yao, hivyo maagizo ya chama kwa serikali, watafute fedha popote wanapojua na suala la kununua mahindi liendelee kwenye maeneo yote ya uzalishaji.” Ameelekeza Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo.

Aidha, katika Hatua nyingine, baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wakulima kuhusu uchache wa vituo vya ununuzi wa mahindi, Chama kimeilekeza serikali kupitia Wizara ya Kilimo, kuongeza vituo vya ununuzi na gharama za usafiri wasibebeshwe wakulima kama inavyofanyika sasa kwa wakulima waliopo pembezoni mwa vituo vya ununuzi.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu ameitaka Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha na Mipango kukutana haraka kwa ajili ya kuangalia namna ya kupunguza mzigo kwa wakulima baada ya ongezeka kubwa la bei ya mbolea kutoka shilingi elfu 50 kwa mfuko wa kilogram 50 na sasa kupanda mpaka shilingi elfu 80-85 katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania kutokana na athari za janga la Uviko 19.

Imetolewa na;

Said Said Nguya
Afisa Habari
Ofisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

Simba SC yasajili 31 CAF
Wadanganyifu mitihani darasa la saba waonywa