Serikali imetoa muda wa mwezi mmoja (kuanzia Septemba 4 hadi Oktoba 4, 2019) kwa wananchi wote wanaomiliki meno ya Tembo kinyume cha sheria, kuhakikisha wanayasalimisha kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na kwamba watakaofanya hivyo kabla ya kuisha kwa muda huo hawatashtakiwa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es salaam mara baada Kikosi Kazi cha Taifa dhidi ya Ujangili (NTAP) kukamata watuhumiwa 8 wa ujangili, vipande 338 na meno mazima ya Tembo 75 pamoja na meno mawili ya kiboko.
“Nimewaita hapa ili mshuhudie kazi nzuri iliyofaywa na maafisa wa Serikali na Kikosi Kazi maalum cha kudhibiti ujangili, ninatoa huruma ya mwezi mmoja kwa kila aliye na meno ya Tembo ayasalimishe kwenye chombo chochote cha Serikali na atakayefanya hivyo ndani ya muda huo hatutamshtaki,”amesema Dkt. Kigwangalla.
Amesema kuwa kukamatwa kwa majangili hao kumetokana na kazi ya muda mrefu ambayo imezaa matunda na matokeo yake kuonekana kwa kukamatwa kwa majangili sugu 8 (nane) akiwemo, Hassan shaban maarufu kwa jina la Nyoni aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa kujihusisha na mtandao wa ukusanyaji wa meno ya Tembo kutoka Tanzania na Msumbiji.
Aidha, amesema kuwa mtuhumiwa huyo wa ujangili amekamatwa na jumla ya vipande vya meno ya Tembo 338 na meno mazima 75 pamoja na meno 2 ya Viboko ambapo kwa mujibu wa Wataalam na Wanasayansi wa Uhifadhi wa Wanyamapori wanaeleza kuwa meno hayo ni sawa na Tembo 117 waliouawa.
Amebainisha kuwa meno hayo yalianza kutafutiwa soko mwaka 2015 wakati Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ilipoingia madarakani, hivyo hatua ya Serikali kuimarisha Ulinzi wa Rasilimali za Taifa na kukiongezea uwezo Kikosi cha Kudhibiti Ujangili soko la meno hayo liliharibika.
Hata hivyo, Dkt. Kigwangalla amesema kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano Majangili wengi wamekamatwa na mitandao yao kusambaratishwa akisisitiza kuwa yeyote atakayejihusisha na biashara hiyo kwa namna yoyote ile atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria.
Dkt. Kigwangalla ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2019 Kikosi Kazi hicho kimefanikiwa kukamata watuhumiwa zaidi ya 1072 silaha 539 zikiwemo silaha 85 za Kivita na jumla ya risasi 37,921.
Aidha, nyara mbalimbali za Serikali zilikamatwa ikiwa ni pamoja na meno tembo, pembe za faru, ngozi za Simba, Chui na Duma, meno ya Kiboko, Kobe pamoja na mazao ya Misitu.
Pia Dkt. Kigwangalla amebainisha kuwa Kikosi kazi hicho hadi sasa kimefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wakubwa wa ujangili wakiwemo Aloyce Francis Ayubu( Kamanda), Mateso Kassiani Albano (Mateso Chupi) na Jayzan George Kuchar (China), Haruna Kassa, Frank Silagei na Ojugu (Original).
Wengine ni Haong Nghia Trung, MS. Yang Feng Glan (Queen of Ivory) ambaye amekwisha hukumiwa pamoja na Salvius Francis Matembo na Manase Julius Philemon, Boniface Maringo, (shetani), Juma Maringo (Yesu), Godfrey James Nyamicha (Papa), Haidari Omary Sharif, Oliva Lucas Mchua na Mrangilwa Emanueli.