Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ameielekeza Bodi ya Korosho kuruhusu usafirishaji wa korosho ghafi nchini kuanzia msimu huu wa 2021/2022 ufanyike kwa saa 24 badala ya saa 12 kama ilivyokuwa katika misimu ya nyuma.
Waziri Mkenda ameyasema hayo leo Agosti 27, 2021 wakati akifungua mkutano mkuu wa wadau wa tasnia ya korosho katika ukumbi wa Benki kuu ya Tanzania tawi la Mtwara, amesema kuwa kwa kufanya hivyo itasaidia kulinda ubora wa zao hilo.
Amesema kuwa Serikali inaendelea kuimarisha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na mfumo thabiti wa upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo ambapo kwa sasa Serikali imeruhusu waagizaji wa pembejeo waagize kadri ya mahitaji ya wakulima badala ya mfumo wa ununuzi wa pamoja ambao ulikuwa na mapungufu kadhaa.
“Tunaposema kazi iendelee, tunamaanisha kila mmoja aendelee kutimiza wajibu wake ipasavyo. Mkulima alime kwa kuzingatia stadi za kilimo; Mnunuzi azingatie taratibu za ununuzi tulizojiwekea; Kiongozi wa Ushirika aendeshe Ushirika kwa uadilifu mkubwa na Msimamizi wa zao (Bodi), awe nahodha wetu kwenye kuimarisha zao husika kwa kuishauri vema Serikali kuhusu namna ya kwenda mbali Zaidi,” Amesema Waziri Mkenda.
Katika hatua nyingine Waziri Mkenda amesema kuwa Changamoto kubwa inayokabiliwa katika sekta ya kilimo nchini ni kupungua kwa tija, ubora na uzalishaji wa mazao hapa nchini ikiwa ni pamoja na zao la korosho.
“Changamoto hii inajidhihirisha kwenye mwenendo wa masoko ya mazao yetu hapa nchini. Njia mojawapo ya kukabiliana na changamoto hii ni kuzingatia kanuni za kilimo bora kama inavyoshauriwa na maafisa ugani wetu kutokana na utafiti wa teknolojia za kisasa za kilimo kutoka kwenye vituo vyetu vya utafiti (TARI),” Amesema Prof Mkenda.
Aidha, Prof. Mkenda amesema kwamba mazao ya biashara yanayotozwa Export Levy ni Korosho peke yake pamoja na biashara ya ngozi ghafi. Hivyo Wizara itaendelea kufuatilia kuhakikisha kwamba Export Levy katika zao la korosho ni lazima irudi ili kusaidia maendele ya zao hilo kama ambavyo ilikuwa imekusudiwa wakati wa uanzishwaji wa tozo hiyo.
Sambamba na hayo yote Waziri Mkenda ameitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Korosho kuhakikisha wanaandaa mpango wa matuzi ya fedha hizo katika kuendeleza zao la korosho.