Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Toshiba nchini Japani, ambapo amewashawishi waje nchini na wafungue ofisi kubwa na waanzishe viwanda vya bidhaa za elektroniki watakavyoona vinafaa hapa nchini.
Ameyasema hayo leo (Jumanne, Agosti 27, 2019) baada ya kutembelea Makumbusho ya Sayansi ya Kampuni ya Toshiba na kiwanda cha kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme cha Tsurumi kinachomilikiwa na Kampuni hiyo.
Akizungumza na viongozi wa kampuni ya Toshiba, Waziri Mkuu amewashawishi waje nchini na wafungue viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali za kielektroniki kama vile redio, televisheni, pasi na viwanda vingine watakavyoona wao vinafaa kujengwa nchini.
Waziri Mkuu amewahakikisha viongozi hao kwamba hawatojuta kuwekeza nchini Tanzania kutokana na sera nzuri na mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara pamoja na soko la uhakika wa bidhaa zitakazozalishwa kwa kuwa Tanzania imezungukwa na nchi nyingi.
“Wawekezaji wote wanaokuja kuwekeza Tanzania wakiwemo na wa kutoka Japan pamoja na kampuni ya Toshiba, watambue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imeboresha mazingira ya uwekezaji na kuyafanya yawe rafiki, nina uhakika wawekezaji watakaoamua kuwekeza Tanzania hawatajutia uamuzi wao huo,”amesema Majaliwa
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Makumbusho ya Sayansi ya Toshiba, Takano Lwakiri amemwambia Waziri Mkuu kuwa Kampuni yake iko tayari kupanua ofisi yake ya Tanzania na kufungua biashara, ambapo ameomba yafanyike mazungumzo yatakayotoa dira sahihi ya kufanikisha jambo hilo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu Mkutano wa Saba wa Tokyo International Conference on Africa Development (TICAD 7) utakaoanza kesho Yokohama nchini Japan, amesema kuwa anaamini kuwa utakuwa na mafanikio makubwa kutokana na ajenda zilizoandaliwa.
Waziri Mkuu amesema miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni pamoja na kuhusu namna ya kuunganisha kibiashara shughuli za Serikali na sekta binafsi.
Amesema kwa kutumia mkutano huo wa TICAD 7 wafanyabiashara wa Tanzania wanayo fursa ya kunufaika kwa kuunganisha nguvu zao na makampuni makubwa ya nchini Japan kama Toshiba ili kupata uzoefu na teknolojia muafaka.
Hivyo, Waziri Mkuu amewasihi wafanyabiashara kutoka Tanzania ambao watashiriki mkutano huo wafanye mazungumzo na wenzao wa Japan, wawashawishi ili waweze kushirikiana nao kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali.
Waziri Mkuu yuko nchini Japan akimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye mkutano wa TICAD 7 utakaoanza kesho, ambapo ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na viongozi wengine wa Serikali na Taasisi za Umma.