Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson leo atakuwa kikaangoni akikabiliwa na maswali ya Wabunge wa ngazi ya juu, huku wadhfa wake ukiwa hatarini kufuatia kujiuzulu kwa Mawaziri wawili muhimu, waliosema hayuko imara kuiongoza Serikali.
Waziri wa fedha, Rishi Sunak na Waziri wa afya, Sajid Javid wamejiuzulu pamoja na mawaziri wengine wadogo, wakisema hawawezi kuendelea kuwa Serikalini kutokana na wingi wa kashfa za utawala wa Johnson katika miezi ya hivi karibuni.
Idadi inayozidi kuongezeka ya wabunge katika chama chake tawala cha Kihafidhina wanasema, wakati umewadia wa Johnson kujiuzulu.
Boris, ambaye ameonekana kujaribu kudhibiti mpasuko katika serikali yake, amemteua Waziri wa zamani wa elimu Nadhim Zahawi kuwa Waziri mpya wa fedha, huku Steve Barclay akiteuliwa kuwa Waziri mpya wa afya.
Upinzani anaopokea Johnson katika chama chake chenyewe, utaonekana wazi baadae leo atakapofika mbele ya Bunge kwa ajili ya kuulizwa maswali.