Wakuu wa nchi za Afrika na wajumbe wa Japan wamekutana katika mji mkuu wa Tunisia, Tunis kwa mazungumzo juu ya kukuza maendeleo ya nchi za Afrika, ambapo Rais wa Tunisia, Kais Saied amewakaribisha wageni kwenye Mkutano huo wa 8 wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD).
Kati wa wageni waliowasili katika nchi hiyo, Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida amepimwa na kukutwa na Covid-19 na kutumia kiunga cha video kujiunga na mkutano huo, unaoongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Macky Sall.
Rais Sall wa Senegal amezungumzia imani yake katika mkutano huo na kusema, “Takriban miaka 30 baada ya kuzinduliwa, Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kwa Maendeleo ya Afrika unaendelea kutekeleza ahadi zake kwa matokeo katika nyanja za elimu, kilimo, afya na maji.”
Ajenda za kikao hicho, ni hatua zinazolenga kukabiliana na ushawishi wa China kwa Afrika ambayo imekuwa ikiongeza ushawishi wake katika miaka ya hivi karibuni, hasa kupitia mradi wake wa “Njia za Hariri”.
Mkutano huo, ni muhimu kwa Taifa la Tunisia wakati huu ambao inaendelea kukumbwa na mzozo wa kisiasa na kiuchumi unaonekana kuwa mbaya zaidi ukiathiriwa na janga la Uviko-19 na vita vya Ukraine vinavyoathiri uagizaji wa ngano.
Tunisia, inatarajia kutumia fursa ya mkutano huo kuvutia wawekezaji wa takriban miradi 80 yenye thamani ya dola bilioni 2.7 katika sekta ya afya, magari, anga na nishati mbadala, ambayo itatengeneza nafasi za kazi 35,700.
Baadhi ya wakuu wa nchi 30 wako kwenye mkutano huo unaoendelea hadi Jumapili, na Tanzania inawakilishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.