Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya kati limeteketeza Vipodozi na bidhaa za Vyakula zilizoisha Muda tani 31.2 vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 katika Dampo la Chidaya jijini Dodoma.

Mkaguzi wa TBS Kanda ya Kati Domisiano Rutahala amesema bidhaa zilizoteketezwa ni kutoka katika Mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora vilivyokamatwa kuanzia Novemba 2021 hadi Agosti 2022.

Mkaguzi wa  Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kati Domisiano Rutahala.

“Wafanyabiashara  tunapowakamata tuna hatua mbalimbali ambazo huwa tunazichukua na zimetaja aina ya faini na hatua za kuchukua, ikiwa ni pamoja na kuzichukua bidhaa hizo na kwenda kuziteketeza,” amesema.

Rutahala amesema bidhaa zilizoteketezwa ni zile zilizoisha muda pamoja na vipodozi vyenye viambata vya sumu kutokana na kuwa na madhara makubwa katika mwili wa mwanadamu.

“Bidhaa za chakula ambazo zimeisha matumizi zina athari kubwa sana mojawapo kutopatikana kwa virutubisho vinavyohitajika pia zinasababisha magonjwa ya muda mrefu na mfupi kama Saratani,” amesema Rutahala.

Tingatinga likitetekeleza bidhaa katika Dampo la Chidaya jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa, “Kwa upande wa vipodozi vina athari kubwa kiuchumi na madhara  ya muda mfupi na mrefu kuathiri mifumo ya macho, ukuaji wa watoto na kina mama wajawazito,”

Mkaguzi huyo wa viwango, amewataka wafanyabiashara wote kuwa makini kwa kufanya ukaguzi wa bidhaa zao na kujiepusha na uuzaji wa bidhaa zenye viambata sumu kutokana na ukubwa wa madhara yake.

Aidha, amewataka wazingatie maelekezo ya utunzaji wa bidhaa hizo ili kuendana na ubora wa uzalishaji.

Kwa upande wa wananchi, Rutahala amewaaasa waepuke kutumia bidhaa zenye viambata sumu na kufanya ukaguzi wa kuangalia  mwisho wa matumizi ili kuepuka madhara.

Waziri Mkuu akutwa na Uviko-19, awekwa karantini
Misaada ya kibinadamu yawekewa 'vigingi' Tigray