Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko aendelee kushughulikia suala la changamoto ya upatikanaji wa nishati ya mafuta katika maeneo mbalimbali nchini.
Majaliwa ametoa maagizo hayo hii leo Septemba 7, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu Bungeni Jijini Dodoma, ambaye alitaka kufahamu ni upi mkakati wa Serikali katika kuhakikisha Taifa linakuwa na mafuta ya kutosha.
Amesema, “Watanzania wapate hii huduma, upatikanaji huu ni muhimu kuhusisha taasisi zote za mafuta na wanunuaji mafuta kwa pamoja ‘bulk’ wakae pamoja na Wizara zinazohusika ikiwemo Wizara ya Fedha na Idara ya Ofisi ya Uratibu Ofisi ya Waziri Mkuu waone namna ya upatikanaji wa mafuta.”
Aidha, Waziri Mkuu ameongeza kuwa, “lakini pia tupanue wigo wa waagizaji wa mafuta ili tuwe na mafuta mengi nchini kwa usalama wa Taifa letu. Na kama hili litafanyika ndani ya wiki moja tutakuwa tumeshapata majibu na kuwapa taarifa Watanzania.Tutahakikisha nishati hii ya mafuta inapatikana na Naibu Waziri Mkuu atashughulikia hilo.”