Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma kuanzisha vitalu vya kuzalisha miche ya Zabibu ili kuwawezesha wakulima kupata mbegu kwa uhakika.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumanne (Julai 06, 2021) alipokua akizungumza na wadau wa uendelezaji wa zao la Zabibu Jijini Dodoma, ambapo amesema vyama vya ushirika wa kilimo cha zao hilo kuanzisha pia vitalu hivyo ili kuwawezesha wananchama kupata mbegu bora.
Pia Waziri Mkuu ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo chake cha Makutupora iimarishe utafiti wa zao hilo, ili kupata miche bora na yenye tija na kuifikisha kwa wakulima,
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kupitia kampeni ya kuendeleza zao hilo, Serikali itasimamia kuhakikisha zao la Zabibu linayolimwa nchini linakuwa na ubora wa hali ya juu, lengo likiwa ni kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi.
Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kwa sasa Wizara ya Kilimo imeanza usajili wa wakulima wa zabibu ili waweze kuwatambua na kuwafikia kwa urahisi.
Amesema mbali na usajili wa wakulima, pia wizara hiyo imeanza majadiliano ya kuanzisha mfuko wa maendeleo ya zao hilo ambao utachangiwa na wenye viwanda na wakulima.
Wakulima wa zao hilo wameiomba Serikali iwasaidie katika upatikanaji wa pembejeo, mikopo pamoja elimu ya namna bora ya kulima zao hilo ili waweze kuongeza tija katika uzalishaji wao.