Kocha Msaidizi wa Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC, Seleman Matola amesema mchezo wa kesho Jumatano (Julai 07) dhidi ya KMC FC hautakuwa rahisi, kutokana na wapinzani wao kuwa na kikosi imara, ambacho kinaweza kupambana muda wote.

Matola amesema licha ya kutarajia upinzani kutoka kwa KMC FC, bado wanaamini kikosi chao kitaweza kufanya kitu ili kufanikisha lengo la kuondoka na alama tatu muhimu.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari leo mchana jijini Dar es salaam, Kocha huyo mzawa amesema wamejiandaa vizuri kwa kuzingatia makosa waliyoyafanya kwenye mchezo dhidi ya Young Africans, ambapo walikubali kupoteza kwa bao 1-0, hivyo watahakikisha wanapambana ndani ya dakika 90.

“Haitakuwa mechi rahisi, kutokana na KMC kuwa na wachezaji wazuri na wanaojielewa, lakini tumejiandaa vizuri kutokana na ugumu huo tupate matokeo mazuri na kuweza kuwa Mabingwa wa ligi msimu huu”

“Tumemaliza Mechi yetu ya Derby salama na hakuna Mchezaji yeyote aliye majeruhi, wachezaji wetu wote wapo kambini, na wapo tayari kwa ajili ya Mchezaji huo wa kesho dhidi ya KMC”

“Tumeangalia makosa yetu na tumeyafanyia kazi. Harafu toka kipindi ligi inaanza kila timu inatafuta Ubingwa kwa hiyo siyo kwamba tunafungwa tunapenda hapana,” amesema Matola

timu hizo zilipokutana kwenye mzunguuko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba SC iliibanjua KMC FC bao 1-0.

Kwa sasa Simba SC inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuwa na alama 73, huku KMC FC ikishika nafasi ya sita kwa kumiliki alama 42.

Mwepu kucheza England
Waziri Mkuu atoa agizo Halmashauri za Dodoma