Klabu ya KMC FC imetangaza vita dhidi ya Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC, kuelekea mchezo wa kesho jumatano (Julai 07) utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

KMC FC watakuwa wenyeji wa mchezo huo, huku dhamira yao kubwa ni kuokota alama tatu dhidi ya Simba SC ambayo ilipoteza mwishoni mwa juma lililopita kwa kufungwa bao 1-0 na Young Africans.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya KMC FC Christina Mwagala amesema, kikosi chao kimejiandaa vya kutosha na wana imani kesho wanakwenda kuibanjua Simba SC ambayo bado inaweweseka na kichapo cha Young Africans.

“Sisi kama Kino Boys hatuwaogopi ila tunawaheshimu kwa sababu tunakwenda kucheza mchezo ambao tulikuwa tunajua kwamba tunakwenda kucheza tarehe 7.”

“Kila mchezaji yupo tayari hivyo mashabiki ninaowamba kesho wajitokeze kwa wingi na jezi za KMC kwa kuwa tupo tayari na tutatoa burudani.”

“Niwahakikishie mashabiki kwamba kesho waje uwanjani na waamini kwamba tunachukua pointi tatu kwa kuwa tutatoa burudani na vitu ambavyo wataviona ni vile ambavyo hawajawahi kuona kwenye mechi zetu za nyuma,” amesema Christina Mwagala.

Mchezo wa mzunguuko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba SC iliibanjua KMC FC bao 1-0.

Simba SC inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuwa na alama 73, huku KMC FC ikishika nafasi ya sita kwa kumiliki alama 42.

Serikali,UNESCO wazindua mradi wa kisayansi
Ndalichako atoa wito kwa wabunifu