Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini waendelee kupiga vita vitendo vya mmomonyoko wa maadili kwa jamii ili kulifanya Taifa kuwa mahali salama kwa watoto na Watanzania kwa ujumla.
Majaliwa ametoa wito huo hii leo Aprili 14, 2023 wakati akifungua Msikiti wa ‘Masjid Ali Bin Saif’ uliopo Vingunguti jijini Dar es Salaam uliojengwa na familia ya Sheikh Seif Ali Seif.
Amesema, moja kati ya msisitizo mkubwa wa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni katika kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto, mmomonyoko wa maadili.
“Tukiachia mmomonyoko wa maadili, tunaweza kutengeneza Taifa ambalo halitakuwa na manufaa mbeleni, Viongozi wa dini mmekuwa mstari wa mbele katika kukemea ukatili dhidi ya watoto,” amesema Waziri Mkuu.
Majaliwa amesema kuwa ni budi kwa Watanzania kuhakikisha wanapiga vita matendo yote yanayoharibu utamaduni, mila na desturi ya mtanzania na kuongeza kuwa, “Tunayoyasikia huko duniani tuombe yasije hapa nchini na kama yapo tuyapige vita.”