Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida na kuwasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kutokana na kifo cha Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Shinzo Abe anayetarajia kuzikwa hapo kesho Septemba 27, 2022.
Akiwasilisha salamu hizo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema “Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatoa pole nyingi kwako, kwa familia ya wafiwa na kwa wananchi wa Japan kutokana na msiba huo.”
Katika mazungumzo yao, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kusisitiza uwepo wa mahusiano mazuri baina ya Tanzania na Japan na kumuahidi nia thabiti ya Serikali ya awamu ya sita ya kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.
Aidha, Majaliwa amekumbushia masuala ambayo walijadiliana kwa njia ya mitandao wakati akiwa Tunisia kwenye mkutano wa TICAD 8, hasa utekelezaji wa miradi ya zamani ambayo Tanzania iliiwasilisha kwenye mkutano wa TICAD 7 inayohusisha ujenzi wa bandari ya Kigoma, mradi wa maji wa Zanzibar na ujenzi wa barabara ya kutoka Arusha hadi Holili mkoani Kilimanjaro.
Miradi hiyo, ni ya ukarabati wa barabara ya Morogoro-Dodoma kwa kiwango cha lami, umwagiliaji katika bonde la Ziwa Victoria, kusambaza maji Lugoda (Mufindi), kujenga uwezo wa kituo cha utafiti cha ufugaji wa samaki Dar es Salaam, bandari ya kisasa ya uvuvi, kuanzisha maabara ya kuthibitisha ubora kwenye sekta ya uvuvi na ukarabati wa bandari ya uvuvi ya Wete na ujenzi wa njia ya umeme ya Somanga-Fungu-Mkuranga.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan amesema watatekeleza ahadi yao ya kuzisaidia nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo ili zijitegemee kwa chakula na kuongeza kuwa, “Kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), watatoa dola za Marekani milioni 300 ili kuzisaidia nchi za Afrika zizalishe chakula kwa wingi na kukabiliana na upungufu wa chakula uliojitokeza baada ya kuzuka kwa vita baina ya Urusi na Ukraine.”