Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezindua Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Kagera wenye lengo la kutangaza fursa za Uwekezaji na hivyo, kukuza maendeleo ya mkoa huo na ameziagiza halmashauri zote za wilaya nchini ziondoe urasimu na kupunguza vikwazo kwa wawekezaji.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Agosti 14, 2019) wakati akizindua Kongamano la Wiki ya Kagera na Mwongozo wa Uwekezaji mkoani Kagera, lilifanyika Bukoba mjini, ambapo amewataka Watanzania wahakikishe wanachangamkia fursa za biashara zilizopo.
Amesema kuwa Watanzania wanauwezo wa kutumia fursa za uwekezaji na biashara zilizopo nchini kwa kushirikiana na taasisi za kifedha na kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini, badala ya kuachia fursa hizo kuchukuliwa na wageni.
“Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda Awamu ya Tatu (2010/2020) na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2015/2016, 2020/2021) ambao lengo lake ni kuendeleza uchumi wa viwanda,”amesema Majaliwa
Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Uwekezaji Kagera, Waziri Mkuu amesema kuwa yamelenga kuwakutanisha wadau wa uwekezaji, ambao ni pamoja na Wafanyabiashara kutoka ndani ya mkoa na nchi jirani zinazozunguka Mkoa wa Kagera.
“Ni ukweli usiofichika kwamba tunahitaji wawekezaji watakaosaidia uchumi wa mkoa huu kukua kwa kasi kupitia fursa zilizopo kwenye nyanja za kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda, maliasili na utalii,”ameongeza
Aidha, amesema kuwa ukuaji mzuri wa uchumi wa mkoa utakuwa na manufaa katika kuongezeka kwa pato la mwananchi wa Kagera, pato la mkoa na hata pato la Taifa nalo litakuwa kwa kasi ndani ya kipindi cha muda mfupi.
Amesema mkoa wa Kagera ndiyo unaoongoza kwa uzalishaji wa Kahawa nchini, ambapo zaidi ya nusu ya Kahawa yote huzalishwa katika mkoa huo. wastani wa uzalishaji wa kahawa kwa mwaka ni kati ya tani 50,000 hadi tani 65,000 kutegemea na hali ya hewa ya mwaka husika.
“Kagera imepakana na Uganda, Rwanda na Burundi. Kupakana na nchi hizo zenye idadi kubwa ya watu katika ukanda huu wanaokadiriwa kufikia takriban milioni 190 ambapo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018 ni fursa ya uwepo wa soko kubwa la bidhaa zinazozalishwa au zinazoweza kuzalishwa katika mkoa wa Kagera,”amesema Majaliwa
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya usafiri ukiwemo wa anga na wa barabara ili kurahisisha usafiri kutoka Bukoba makao makuu ya mkoa wa Kagera kufika katika nchi hizo.
“Kwa mfano, umbali kutoka Bukoba hadi Kampala ni km. 340, Bujumbura km. 550 na Kigali km. 490. Kadhalika, itakuwa ni rahisi kufikia masoko ya nchi za Sudan Kusini pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC),”amesisitiza
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amesema kuwa dhamira ya kuandaliwa kwa wiki ya uwekezaji mkoani Kagera ina lengo la kuhakikisha kwamba mkoa huo unafanya vizuri katika sekta ya uwezekezaji na biashara, hivyo kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.
Kwa upande wao, viongozi mbalimbali wakiwemo Magavana na wafanyabiashara kutoka nchi za Rwanda na Burundi wameahidi kutumia fursa zilizopo nchini, pamoja na kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania kwenda kuwekeza katika nchi zao.