Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Mifugo ziweke utaratibu utakaowafanya wafugaji wafuge kitaalamu badala ya utaratibu wa kuwa na mifugo mingi anayoshindwa kuihudumia.
Majaliwa, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Viongozi na wananchi waliohudhuria kikao cha siku moja cha kukabidhi rasmi mradi wa makazi maalum katika kijiji cha Msomera kwa Wilaya za Handeni na Kilindi za Mkoani Tanga.
“Wizara ya Mifugo pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI tengenezeni taratibu za kuonesha mfugaji wa Msomera mwenye ng’ombe 70 anafuga kwa tija zaidi kuliko mwenye ng’ombe 300. Hii inaweza kutumika hata kwenye mikoa mingine ambako kuna wafugaji,” amesisitiza Majaliwa.
Aidha, pia amezitaka Halmashauri za Mji Handeni na Wilaya za Handeni na Kilindi zinapoandaa bajeti zao kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha, zihakikishe zinaingiza mahitaji ya uendelezaji huduma kwenye kijiji cha Msomera, ili kuimarisha ustawi wa wananchi wa kijiji hicho.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu pia amewataka Mawaziri na Makatibu Wakuu wanapoenda kufanya ziara kwenye kijiji hicho wahakikishe wanaanzia kwanza kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kujitambulisha rasmi ndipo wapatiwe maafisa wa kuongozana nao.