Waziri mkuu mteule wa Iraq Mohammad Allawi amejiondoa katika jukumu la kuunda serikali, hatua ambayo inaitumbukiza nchi hiyo katika sintofahamu ya kisiasa, na kumuacha Rais Barham Saleh na siku 15 kupendekeza Waziri Mkuu mpya, ambaye anaweza akamtaja moja kwa moja bila kushauriana na bunge.
Akiijibu taarifa ya kujiondoa Allawi, Rais Saleh amesema ameanzisha mashauriano ya kumtangaza mtu mwingine katika muda uliowekwa kikatiba.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Allawi amesema alichukua hatua hiyo kwa sababu baadhi ya makundi ya kisiasa hayakuwa makini kuhusu mageuzi, wala kuzitekeleza ahadi zao kwa watu.
Wakati hayo yakijiri, jeshi la Iraq limesema makombora mawili yalilipiga eneo la ubalozi wa Marekani pamoja na kituo cha wanajeshi wa Marekani mjini Baghdad.