Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe leo ametembelea vijana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys walio katika kambi ya mazoezi katika Viwanja vya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari mara alipotembelea kikosi cha timu hiyo, Mwakyembe alisema, vijana watumie uzalendo kuhakikisha wanajiandaa ipasavyo kwa kufuata maelekezo ya makocha wao ili kubakiza kombe nyumbani.
“Naomba vijana wangu jitumeni kwa uzalendo wote, nyie ndiyo mtakaopeperusha bendera ya taifa, tumieni nguvu zote ili kufanya vizuri katika michuano hiyo kwa kuanza maandalizi sasa na kwa upande wetu serikali hatutasita kutumia nguvu zetu zote kuwasaidia kuhakikisha mnafika mbali sana kwani mna walimu wazuri, Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu wake Mama Samia Suluhu wamenituma niwafikishieni ujumbe huu, mna viongozi wa TFF wazuri, hakuna kitakachowashinda.
Poulsen na timu yenu mmebeba dhamana kubwa ya kuhakikisha mnawasaidia vijana hawa kukuza vipaji vyao kwani wanatazamwa na kila jicho la Mtanzania,” amesema Mwakyembe.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa Fainali za Vijana za Afrika chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwakani ambapo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lipo katika mpango wa kuwaandaa wachezaji hao kuelekea katika fainali hizo.Kambi ya awali ya timu hiyo itaisha Januari 28, mwaka huu kisha watakuwa wakikutana kila mwezi kabla ya kushiriki michuano ya Cecafa itakayofanyika Agosti, mwaka huu.