Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema njama zinazofanywa na watu wasio waaminifu huku wakihakikisha wanazingatia sheria na taratibu ili wasibainike, ni tatizo kubwa linalosababisha thamani ya fedha kutopatikana kwenye miradi.
Ameyasema hayo leo, Mei 26, 2021, jijini Dodoma alipokuwa akifungua Kongamano la Nane la Mwaka la Usimamizi Katika Ununuzi wa Umma, lililoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), ambapo washiriki ni Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi za taasisi nunuzi, Maafisa masuuli, Mameya na Wenyeviti wa Mabaraza ya Madiwani ya Halmashauri pamoja na Madiwani.
Dkt. Nchemba amesema watu hao wenye uwezo wa kufanya njama kwa kiwango cha juu, huingiza njama zao kuanzia hatua za awali za michakato.
“Kuna njama kwenye michakato ya ununuzi wa umma. Ukifuatilia unakuta watu wamezingatia sheria na taratibu, lakini ndani yake kunakuwa na njama,” alisema Dkt. Nchemba.
“Wengine wanatengeneza njama kuanzia wazo la mradi linapoanzia. Njama hiyo inaenda hadi kwenye bajeti ya Serikali inaingia. Wakati Waziri anawasilisha bajeti ya Serikali, unakuta watu wanashangilia kweli, unadhani labda waziri alitoa bajeti nzuri, lakini kumbe wao wanasherehekea njama yao imepita pia,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Fedha na Mipango alitoa onyo kwa watendaji wa Serikali wasio waadilifu, hususan wanaohusika katika michakato ya ununuzi wa umma.
Alisema ili wananchi wapate maendeleo endelevu kama ambavyo Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inavyokusudia na kuweka juhudi katika utekelezaji wa miradi, ni lazima uzingatiaji wa sheria na taratibu uende sambamba na uadilifu.
“Nitoe rai kwa watekelezaji wa miradi yote, kama tunataka kupiga hatua katika taifa letu, kila mmoja anapaswa kushiriki. Ushirikiano uanze kwa kila mmoja wetu, na kila mmoja awe ni mlinzi wa mwenzake,” alisema.
Aidha, Dkt. Nchemba aliwasihi washiriki wa kongamano hilo lenye Kauli Mbiu, ‘Maboresho ya Mfumo wa Ununuzi wa Umma Nchini Tanzania: Mafanikio na Changamoto zake’ kufuatilia kwa makini mijadala na maazimio ya kutatua changamoto za sekta ya ununuzi wa umma.
Pia, aliwataka washiriki kuhakikisha wanayaishi maazimio ya kongamano hilo kwa maslahi mapana ya Taifa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Balozi Dkt. Matern Lumbanga ametoa rai kwa wadau wote wa ununuzi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kuzingatia sheria ya ununuzi wa umma, kwakuwa hilo sio suala la hiari.
Balozi Lumbanga alimhakikishia Waziri Nchemba kuwa PPRA itaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali kuhakikisha kuwa inatekeleza majukumu yake ya kusimamia sheria ya ununuzi wa umma.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Leonard Kapongo, alisema Mamlaka hiyo imeisaidia Serikali kuokoa takribani shilingi bilioni 30 (30bn/-) ambazo zingepotea kutokana na kutofuatwa kwa taratibu za ununuzi na hasa katika eneo la usimamizi wa mikataba, katika Mwaka wa Fedha 2017/18 hadi 2019/20.
“Sehemu ya fedha zilizookolewa zinatokana na malipo wakandarasi na watoa huduma kinyume na utaratibu na hivyo taasisi hizo kuelekezwa kurejesha fedha hizo,” alisema Mhandisi Kapongo.
Aidha, Mhandisi Kapongo aliwataka washiriki wa kongamano hilo na wananchi kwa ujumla, kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa.
Aliongeza kuwa kwa kuzingatia kuwa rushwa husababisha kutopatikana kwa thamani ya fedha kwenye ununuzi wa umma, PPRA imeshirikiana na Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuandaa na kusambaza Mwongozo wa Kuzuia Rushwa katika Ununuzi wa Umma.
Hivyo, aliwataka watendaji wa taasisi zote kuhakikisha wanautumia muongozo huo muhimu ili kupambana na vitendo vya rushwa.
PPRA imeandaa kongamano hilo linalofanyika katika majiji mawili nchini, yaani Dodoma (Mei 26-27, 2021) na Arusha (Juni 1-3, 2021).
Awamu ya pili itakayofanyika jijini Arusha, washiriki ni Wajumbe wa Bodi za Zabuni, Wakuu na Watendaji katika Vitengo vya Usimamizi wa Ununuzi, Vitengo vya Sheria, Wakaguzi wa Ndani na Idara Tumizi.