Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ametangaza vita dhidi ya watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini wakivusha kwa njia za panya kupitia maeneo ya mipakani.

Waziri Nchemba jana alitoa siku 14 kwa Jeshi la Polisi na maafisa wanaohusika kudhibiti biashara ya dawa za kulevya, kuwatia nguvuni watu wanaojihusisha na biashara hiyo katika mpaka wa Tunduma, wanaodaiwa kusafirisha kwa njia ya panya hadi nchini Zambia na nchi nyingine jirani.

Alisema kuwa Tanzania imekuwa ikichafuliwa na watu wanaofanya biashara ya dawa za kulevya kiasi kwamba katika baadhi ya nchi ukijitambulisha kuwa ni Mtanzania hujikuta ukiongezewa baadhi ya masharti kutokana na uzoefu wa Watanzania wengi kukamatwa na dawa za kulevya.

“Hatuwezi kuacha nchi ikachafuka kwa sababu tu ya watu wachache.Ukienda China Watanzania zaidi ya 200 wanashikiliwa kwa dawa za kulevya, Pakistan wapo, India, Afrika Kusini ni Watanzania. Hili linatuchafua sana,” alisema.

Alisema kuwa mpaka huo ni maarufu kwa biashara hiyo na kwamba wapo watu ambao sio wafanyakazi wa mabasi lakini wamekuwa wakisafiri kila siku na mabasi hayo wakipitisha mizigo na kuishuka kwenye vijiji kadhaa kwa ajili ya kusafirishwa kwa njia ya panya.

Waziri huyo alilitaka Jeshi la Polisi kuwasiliana na Mamlaka za nchi jirani ili washirikiane kukomesha biashara hiyo haramu inayofanywa katika mpaka huo.

Video: Zlatan Ibrahimovic alivyo dhihirisha ubora wake Man U
Video: Itazame Chapaa ya GentrIez ft. Belle 9 na Young Dee