Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ummy Mwalimu amekemea utozaji wa michango mbalimbali kwa wanafunzi shuleni sanjari na vitendo vya baadhi ya walimu kuwazuia wanafunzi kuingia shuleni kwa kukosa sare na mahitaji mengine yanayohitajika shuleni hapo.
Amesema vitendo hivyo havikubaliki na kwamba walimu hao wanapaswa kuwa na huruma kwa wazazi na walezi wa watoto hao na kwamba wanapaswa kuhakikisha wanaepuka kuwakwamisha watoto hao kusoma.
“Walimu wasiweke vikwazo kwa watoto wanaoanza darasa la kwanza, Katibu Mkuu hakikisha unaandika waraka wa utaratibu, tunataka shule zinapofunguliwa Januari watoto 907,802 wa kidato cha kwanza wanaanza shule” Amesema Waziri Ummy
Katika kulisisitiza hilo Waziri Ummy amesema anatafuta shule mbili au tatu za kutolea mfano endapo zitabainika kutenda kosa hilo na kusisitiza kuwa wazazi hawapaswi kubebeshwa mzigo kwa kuwa Serikali ilishaweka utaratibu wa elimu bila Ada.
Waziri Ummy ametoa kauli hiyo Mkoani Dar es Salaam alipomwakilisha Rais Samia Suluhi Hassan katika ufunguzi wa Mkutano wa 16 wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) ambapo pamoja na mambo mengine aliwapongeza walimu hao kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa madarasa unaoendelea nchi nzima.
“sitaki kuona mwanafunzi amerudishwa kwa sababu ya michango na kwa hawa wanaonza kidato cha kwanza hata kama hawana sare ya shule aliyochaguliwa asirudishwe bali apewe muda,” Amesema Waziri Ummy.
Awali Katibu Mkuu wa Tahossa Titus pamoja na mafanikio mbalimbali aliyoyabainisha, alisema Tahossa bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwepo ya ucheleweshaji wa fedha za mpango wa bila malipo shuleni hali inayozifanya shule kushindwa kutatua baadhi ya mambo.
Amesema ukiacha hilo na mengine elimu ya sekondari imeendelea kupata mafanikio makubwa kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali siku hadi siku huku akiishukuru Serikali kwa namna ambavyo inajitoa kuhakikisha sekta ya elimu inapiga hatua.