Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Ummy Mwalimu leo Decemba 22, 2020 amefanya ziara ya kikazi visiwani Zanzibar ambapo amekutana na Rais wa Zanzibar pamoja na Makamu wa kwanza wa Rais Maalim Seif.
Waziri Ummy amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi Ikulu Zanzibar.
Katika mazungumzo yao Mwalimu amesema kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais – Zanzibar amedhamiria kuendeleza jitihada za kutatua changamoto za Muungano zilizobakia.
“Rais nikuhakikishie kuwa nitafanya kazi kwa karibu sana na Khalid Waziri kuhakikisha hoja ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi zinafanyiwa kazi na mwanzoni mwa mwezi Januari tunategemea kuwa na kikao cha pamoja baina yetu” Amesema Ummy.
Aidha Rais Mwinyi amempongeza Ummy Mwalimu kwa kuteuliwa tena kuwa Waziri na kusisitiza kuwa Serikali yake itampa ushirikiano katika kuratibu masuala ya Muungano.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy Mwalimu amefanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharrif Hamad Chukwani Zanzibar.
Maalim Seif, amesisitiza umuhimu wa Wizara zenye hoja za Muungano kukutana na kutafuta suluhu ya mapema na kuhamasisha Wizara zisizo na hoja kukutana pia kwa lengo la kudumisha undugu baina ya Tanzania bara na Tanzania Zanzibar.
“Nashauri na kusisitiza Wizara zinazoshabihiana zikutane na kuhakikisha hoja zinazopatiwa ufumbuzi zitekelezwe ipasavyo” amesema Maalimu Seif Sharif Hamad.