Waziri wa afya na mbunge wa chama cha Conservative nchini Uingereza Nadine Dorries amethibitisha kukutwa na maambukizi ya virusi vya corona.
Dorries ambaye ni mbunge wa kwanza kugundulika na maambukizi, alichukua tahadhari zote baada ya kubaini kuwa ameathirika, na amejiweka karantini nyumbani kwake.
Hali hii imekuja wakati kukiwa na taarifa ya kifo cha mtu wa sita kutokana na virusi vya corona nchini Uingereza ambako kuna visa vya watu 382 kuambukizwa.
Mtu aliyepoteza maisha hivi karibuni ni mzee mwenye umri wa miaka 80 ambaye alikuwa na changamoto za kiafya.
Wakati huohuo hospitali kuu Uingereza imesema inaboresha uwezo wake wa kuwapima watu, wakati idadi ya maambukizi ikitegemewa kuongezeka.
Mawaziri wote wa afya, akiwemo Waziri Mkuu wa afya Matt Hancock, watafanya vipimo, sambamba na maafisa wengine ambao walikaribiana na waziri Dorries.
Idadi ya watu walioambukizwa nchini Uingereza ni 324 England, 27 Scotland, 16 Ireland Kaskazini na 15 Wales. Watu 91 jijini London, huku Kusini-Mashariki, kukiwa na visa 51.
Ofisi ya mambo ya nje ya Uingereza imewataka raia kufanya safari zilizo muhimu pekee kwenda Italia, ambayo ina maambukizi makubwa zaidi baada ya China.
Raia wa Italia wameamriwa kubaki nyumbani, na kuomba ruhusa kwa safari muhimu.
Idara ya mambo ya nje imeshauri kuwa mtu yeyote anayewasili Uingereza kutokea Italia tangu siku ya Jumatatu, ajiweke karantini kwa siku 14.