Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Kirstjen Nielsen, amejiuzulu Jumapili jioni kufuatia mkutano aliofanya na Rais Donald Trump Ikulu mjini Washington DC.
Kupitia ujumbe wa Twitter, Trump amesema Nielsen ataiacha nafasi hiyo na kumshukuru kwa huduma yake.
Trump pia ametangaza kwamba Kamishna wa forodha na ulinzi wa mipakani, Kevin McAleenan, atakaimu nafasi iliyoachwa wazi na Nielsen.
Nielsen, mwenye umri wa miaka 46, aliteuliwa kama waziri wa Usalama wa Ndani mwezi Oktoba 2017 na kuapishwa tarehe 6 mwezi Desemba mwaka huo.
Alikuwa waziri wa sita tangu wizara hiyo kubuniwa na waziri wa pekee mwanamke aliyekuwa amesalia kwenye baraza la mawaziri la Trump.
Kujiuzulu kwake kunajiri wakati ambapo Rais Trump anakabiliwa na tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu kupitia sera zake za uhamiaji, hususan kuhusu wahamiaji kutoka mataifa ya Amerika ya Kati na Kusini.
Nielsen aliandamana na Rais Trump Ijumaa mjini Calexico, California, wakati rais huyo alipokagua ukarabati wa ukuta kati ya Marekani na Mexico.
Wakosoaji wake walimshutumu kwamba hakuonyesha utu kwa baadhi ya familia zilizokuwa zikijaribu kuvuka mpaka kuingia Marekani lakini baadhi ya wachambuzi wamesema kuwa Rais Trump hakuwa na imani Nielsen angetekeleza sera za uhamiaji kwa kasi ambayo alitaka.
Trump ameelezea nia yake ya kufanya mageuzi makubwa katika wizara hiyo ya Usalama wa Ndani na kutishia kufunga mpaka kati ya Marekani na Mexico iwapo nchi hiyo haitashirikiana katika kuwazuia wanaoomba hifadhi Marekani.