Wakazi wa eneo la Mto wa Mbu Wilayani Monduli Arusha, wameuzuia msafara wa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wakilalamikia kukosa huduma muhimu ya maji, ambapo Waziri huyo ametangaza kuzivunja Jumuiya za Watumia Maji wa eneo hilo kwa kushindwa kutekeleza majuku yao.
Wakazi hao, wamemueleza Waziri Aweso kwamba kumekuwepo na upendeleo wa ugawaji wa huduma ya maji yanayopatikana kwa shida ambapo wafanyabiashara wenye Hoteli wamekuwa wakipewa kipaumbele.
“Kamati za Maji ndio zimekuwa zikifanya kazi ya kupeleka maji kwa wafanyabiashara huku taasisi zikiwano shule zikinyimwa maji na hii inasababisha ugumu wa mambo muhimu nyumbani, makazini na hata kwa wanafunzi shuleni,” walisisitiza Wakazi hao.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Serikali iliagiza Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), wayaanishe maeneo yote yenye changamoto ili yapatiwe ufumbuzi na kumtaka Meneja wa RUWASA Mkoa wa Arusha, Joseph Makaidi kutoa maelezo kwa wananchi.
Akiongea mbele ya Waziri, Meneja huyo amesema zaidi ya Shilingi 1.7 Bilioni zimetengwa kwa ajili ya kumaliza tatizo sugu la maji katika eneo la Mtowambu, na kwamba bado wanakamilisha taratibu za manunuzi ili kumtangaza mzabuni.