Mamlaka za Usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – DRC, zinasema idadi ya wanaosadikika kufariki kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo imeongezeka na kufikia watu 176.
Mamlaka hiyo, imebainisha kuwa watu zaidi bado hawajulikani walipo na wanahofiwa kufukiwa chini ya udongo huku shughuli za uokozi zikiendelea kufanyika, hali ya tahadhari kutolewa na juhudi za msaada zikifanywa.
Aidha, inaarifiwa kuwa Vijiji vya Bushushu na Nyamukubi – vilisombwa na maji baada ya mito ya mashariki mwa Congo kuvunja kingo zake nankusababisha maporomoko makubwa ya udongo ambayo yaliharibu nyumba nyingi.
Hata hivyo, taarifa za vyombo mbalimbali vya Habari zinasemq katika moja ya vijiji zaidi ya robo tatu ya nyumba zote zimesombwa na maji ikiwa ni pamoja na vituo vya afya na shule.
Madhara haya yanaripotiwa ikiwa tayari upande wa pili wa Ziwa Kivu katika nchi jirani ya Rwanda kumetokea vifo vya takriban watu zaidi ya 130 kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyoacha simanzi na majonzi kwa raia wengi.