Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa, Alice Cruz kupitia wa ripoti yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema Watu wenye ukoma, wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu, ili haki zao za kuwa na ulemavu ziweze kutambuliwa kitaifa na kimataifa.
Mtaalamu huyo maalum, wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ukoma amesema watu walioathiriwa kwa ukoma wanapaswa kutambuliwa kikamilifu kuwa wana ulemavu.
Amesema, kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa watu wenye ulemavu, CRPD unaonesha kuwa ulemavu wao wa viungo umesababishwa na ukoma, na kwamba unyanyapaa wanaokabiliana nao umetokana na fikra potofu za ukoma.
Ameongeza kuwa, wanafamilia wa mtu mwenye ukoma, nao pia hujitambulisha kuwa ni watu wenye athari za ulemavu wa kisaikolojia, kutokana na unyanyapaa na ubaguzi kwa msingi wa kuishi na watu wenye ukoma.
Hata hivyo amesema, pamoja na kutambua hatua katika ngazi ya kitaifa ya kuweka usawa kwa watu wenye ukoma na wale wenye ulemavu, bado anataka hatua zaidi zichukuliwe ili kutekekeleza kwa kina vipengele vilivyomo kwenye mkataba wa watu wenye ulemavu.
Cruz, pia ametaka serikali ziongeze maradufu harakati zao za kulinda na kusongesha haki za watu walioathirika kwa ukoma na familia zao, kwa kutambua haki zao na washiriki kwenye utungaji wa sera.