Klabu za West Ham Utd na Tottenham zote za jijini London, zimefunguliwa mashataka na chama cha soka nchini England (FA), baada ya kubainika mabenchi ya ufundi ya pande hizo mbili yalishindwa kuzuia hasira za wachezaji wao, wakati wa mchezo wa ligi kuu uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita.
Taarifa iliyotolewa na FA imeeleza kuwa, “Kutokana na fujo zilizohusisha wachezaji wa klabu za West Ham Utd na Tottenham katika dakika 95 ya mchezo, zinakabiliwa na mashataka ya kujibu kutokana na wahusika wa mabenchi ya ufundi kushindwa kuzuia ghasia hizo.”
Klabu hizo zimepewa muda wa kuwasilisha utetezi wa mashtaka yanayowakabili hadi kesho saa kumi na mbili jioni kwa saa za England, kabla ya hukumu ya mwisho haijatolewa na FA.
Wachezaji watano walionyeshwa kadi za njano na mwamuzi Michael Oliver kutokana na zogo hilo lililoibuka kabla ya kipyenga cha mwisho kupulizwa.
Upande wa West Ham Utd walioonyeshwa ni Andy Carroll, Winston Reid na Andre Ayew huku Eric Dier na Fernando Llorente wakiadhibiwa upande wa Spurs.
Vurugu hizo ziliibuka baada ya mshambuliaji wa West Ham Andy Carroll kuangushwa kwa kukwatuliwa, jambo ambalo lilimpa hasira na kumrudia aliyemfanyia hivyo.
Spurs ambao walikua wageni katika mchezo huo, hawakupendezwa na hali hiyo, hasa baada ya kuwa pungufu kufuatia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa beki wao wa pembeni Serge Aurier dakika 20 kabla kipyenga cha mwisho.
Katika mchezo huo Spurs waliibuka wababe kwa ushindi wa mabao matatu kwa mawili.