Shirika la Afya Duniani WHO, limesema lina matumaini litapata mwaliko China ili kushiriki katika uchunguzi wa kubaini virusi vya corona vinavyosababisha homa ya mapafu vilitoka kwa wanyama gani.
Msemaji wa shirika hilo, Tarik Jasarevic, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba shirika lake litakuwa makini kufanya kazi na washirika wa kimataifa, katika uchunguzi huo ikiwa kutakuwa na mwaliko kutoka kwa serikali ya China.
Hata hivyo ameongeza kuwa shirika lake halijashiriki katika uchunguzi wowote unaoendelea China kwa sasa.
Amesema kuwa shirika hilo linafahamu kuwa kuna chunguzi kadhaa zinazoendelea nchini China kwa lengo la kuboresha uelewa kuhusu chimbuko la mlipuko wa Corona.
Wanasayansi wanaamini kwamba kirusi hicho hatari kilitoka kwa wanyama na kuwaambukiza wanadamu.