Mshambuliaji Wilfried Bony amekiri kuchukizwa na kitendo cha cha kutocheza michezo kadhaa akiwa na klabu ya Stoke City, iliyomsajili kwa mkopo mwanzoni mwa msimu huu akitokea Man City.
Bonny mwenye umri wa miaka 28, hajacheza katika kikosi cha kwanza cha The Potters tangu Disemba 27, huku ikiwa tayari ameshaifungia Stoke City mabao mawili kwenye michezo 11 aliyocheza.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Ivory Coast amesema ni vigumu kuamini kama anashindwa kutumika katika kikosi cha kwanza tangu mwishoni mwa mwaka jana, ukilinganisha na juhudi anazozionyesha mazoezini.
Hata hivyo Bonny anajutia maamuzi ya kukataa kwenda nchini China wakati wa majira ya baridi (Mwezi Januari) kwa kuamini huenda hali ya kukalishwa benchi ingebadilika.
Mkataba wake wa mkopo klabuni hapo, unamruhusu Bonny kuondoka na kwenda kokote endapo atapata ofa, na ilipotokea bahati ya kuhitajika huko mshariki ya mbali aligoma na kusisitiza anataka kubaki England.
“Wakala wangu aliniambia kuhusu ofa iliyotumwa kutoka china, lakini nilimkatalia na biashara hiyo haikufanyika, niliamini bado ninaweza kucheza hapa na kuonyesha kiwango kikubwa cha soka langu, lakini leo imekua tofauti.”
“Ninashangazwa na hali hii, maana ninafanya mazoezi, na meneja ananiambia kila leo nipo vizuri na nina nidhamu ya kutosha, lakini linapokuja suala la kucheza inakua ngumu kwangu. Alisema Bonny.