Muigizaji na mwanamuziki mkongwe, Will Smith ameonekana kumpiga kofi mchekeshaji Chris Rock kufuatia utani alioutoa kumuhusu mke wake, Jada Pinkett Smith, katika usiku wa utolewaji wa tuzo za Oscar.
Ni katika Saa ya tatu ya kipindi cha runinga, ambapo Rock alipanda jukwaani kuwasilisha tuzo ya filamu bora zaidi, na akatoa mzaha kuhusu kichwa cha Pinkett-Smith kwa kusema alikuwa kwenye GI Jane 2- akionekana kurejelea mfano wa kichwa chake kilichonyolewa.
Hii ni kufuatia uamuzi wa Pinkett-Smith kuweka wazi siku za nyuma kuhusu kusumbuliwa na tatizo la ‘alopecia,’ hali inayosababisha nywele kukatika zenyewe.
Baada ya Rock kutania hivyo, Will Smith akatamka kwa sauti ya juu “Ondoa jina la mke wangu kinywani mwako” mara mbili wakati matangazo hayo yakiwa yamesitishwa kwenye televisheni kwa watazamaji wa nchini Marekani.
Baada ya kutamka hivyo, Smith alikimbilia jukwaani na kumpiga Rock kofi, na kuonekana kumshtua Rock, akimuacha anacheka huku akiongea maneno ya kuendelea kuchekesha.
Hii si mara ya kwanza kwa Rock kumtaja Pinkett-Smith kwenye tuzo za Oscar, Ikumbukwe mnamo mwaka 2016, mara ya mwisho Rock aliandaa sherehe hiyo, ambapo alizunguzia kuhusu, “Jada Pinkett Smith kugomea tuzi za Oscars ni kama mimi kugomea suruali ya Rihanna – sikualikwa.”
Akiongeza mafuta kwenye moto huo, Scott Feinberg, mkosoaji aliyehudhuria sherehe hiyo, alitweet kwamba “wakati wa mapumziko ya kibiashara, Will Smith anawekwa kando na kufarijiwa na Denzel Washington na Tyler Perry, ambao walimwomba alipuuze suala hilo.
Wakati wa tukio hilo walikuwepo pia nyota wengine walioonyesha kushtushwa na kitendo hicho akiwamo Lupita Nyong’o, aliyeketi nyuma ya Smith.
“Najua kufanya kile kilichotokea lazima ichukuliwe kama unyanyasaji, watu kuzungumza juu yako na kuwa na watu wanaokudharau, unapaswa kutabasamu na kujifanya kuwa sawa,” alisema Smith, akionekana kuthibitisha kwamba tukio la kumchapa kofi Chris Rock halikuandikwa bali lilitokana na maumivu ya kweli.
Smith alisema kabla tu ya ushindi wake, Denzel Washington alimwambia: “Wakati wako wa juu zaidi, kuwa mwangalifu, hapo ndipo shetani anakuja kwa ajili yako, Nataka kuwa chombo cha mapenzi, Nataka kuwa balozi wa aina hiyo ya upendo, utunzaji na kujali. Nataka kuomba radhi kwa Academy na wateule wenzangu wote.” Smith alisema huku akitokwa na machozi.
Baadae Will Smith alishinda tuzo ya mwigizaji bora kwa nafasi yake kama Richard Williams, baba wa Venus na Serena, katika katika filamu maarufu King Richard.