Na Abdulah Mkeyenge
JINA kamili ni Jack Andrew Garry Wilshere. Jina maarufu Jack Wilshere. Stori yake ya maisha ya soka inasisimua. Wilshere ana miaka 28. Yuko na ‘Wagonga Nyundo wa London’ West Ham United.
Wilshere ni product za mwisho mwisho za mzee Arsene Wenger kabla hajatupa taulo. Kinachomtokea sasa Wilshere, sidhani kama Wenger anakifurahia huko aliko. Moyo wake utakuwa unapondeka pondeka. Unamuuma sana.
Wenger na dunia iliamini Wilshere anakuja kuwa mrithi wa Xavi Hernandez, Andrea Pirlo katika eneo la dimba, lakini haikuwa hivi badala yake Wilshere amekuwa mchezaji wa kawaida anayeandamwa na majeraha ya kila mara. Hata akipona haonyeshi kurejea kule ambako Wenger na dunia iliamini angefika.
Wilshere amewahi kucheza na viungo mahiri na kujipambanua tena katika viwanja vigumu. Amewahi kutamba Camp Nou katika ngome ya Hernandez na pacha wake Andres Iniesta wakiwa kiwanjani na Wilshere akawatawanya. Amewahi kucheza na Yaya Toure pale Etihad na kumtawanya. Yuko wapi Wilshere huyu?
Katika umri wake alipaswa kuwa moja ya nahodha wa timu kubwa, lakini badala yake katika umri huu amekwenda kuwa mchezaji wa kawaida katika timu ya kawaida.
Wilshere amejipoteza mwenyewe kwa mambo yake ya nje ya uwanja. Alianza kujipoteza hapa. Umri wake ndiyo wachezaji wanachanganya kutokana na kukomaa, lakini kwake haiko hivi. Yuko West Ham katika picha ya kivuli, lakini picha yake halisi ameiacha Arsenal.
Wilshere alikuwa mgumu, mbishi, anacheza tafu, mwisho kabisa miguu yake ilibalikiwa kipaji. Hakuwa kiungo wa kawaida, alikuwa kiungo kweli, lakini amejipoteza mwenyewe kwa mambo yake ya kipuuzi. Mara kadhaa tumewahi kuziona picha zake za utupu zikizagaa mitandaoni, muda mwingine tukaona picha zake akiwa anavuta sigara, huku amezungukwa na kundi la wanawake, muda mwingine tukaona picha zake akipigana baa, unakuwaje mchezaji mwenye sifa mbaya zisizovutia kama hizi bado ukaenda kiwanjani na uktamba? Ni ngumu na ndiyo maana hata mwisho wake ulitabirika kiurahisi.
Moja ya rafiki zangu Peter Kadutu alimpenda Wilshere na kuniambia akipata mtoto wa kiume angemuita jina hili. Amepanga kufanya hivyo kama kunilipizia mimi niliyemuita mtoto wangu jina la Drogba. Sijui kama mpaka sasa Kadutu ana ndoto hii. Sijui. Kuna siku nitakuja kumuuliza.
Katika nyakati hizi tulipaswa kuishuhudia battle ya Ngolo Kante na Wilshere, Jordan Henderson na Wilshere, lakini haiko hivi. Badala yake nafasi yake sasa pale Arsenal wamekuja wachezaji wengine waliokosa moyo wa Simba uliojaa ujasiri kama wake. Amejimaliza mwenyewe.
Leo hii yuko West Ham, lakini kama hayuko. Kumbukumbu pekee aliyotuachia ni ule mchezo wa Barcelona na Arsenal uliopigwa pale Nou Camp.
Siku ile Wilshere alikuwa katika kilele cha ubora wake, alipishana vyema na kina Hernandez na Iniesta ambao ukicheza nao Camp Nou inahitajika nguvu, akili ili kuwazima, lakini Wilshere aliweza kuwazima!