Rapa Wiz Khalifa ametimiza ndoto yake baada ya kuvunja rekodi ya YouTube baada ya video ya wimbo wake ‘See You Again’ kuwa video iliyotazamwa zaidi tangu kuanzishwa kwa mtandao huo wa video.
Wiz amefunika rekodi ya wasanii wote duniani akiipiku video ya ‘Gangnam Style’ ya mwimbaji wa Korea Kusini, PSY. ‘See You Again’ imefanikiwa kuangaliwa zaidi ya mara bilioni 2 na laki tisa (2,907,015,128) huku Gangnam Style ikifuatia kwa kutazamwa mara 2,894,970,917.
‘See You Again’ ni wimbo ulioachiwa miaka miwili iliyopita maalum kwa kumbukumbu ya muigizaji wa filamu ya Fast and Furious, Paul Walker aliyefariki kwa ajali ya gari. Kiitikio cha wimbo huo kilifanywa na Charlie Puth.
“Ninafuraha kubwa na ninamshukuru kila mmoja ambaye aliunga mkono wimbo na video hii YouTube. Ninafurahi kuhamasisha maisha ya watu wengi,” amesema Wiz Khalifa.
- Justin Bieber awakera mashabiki wimbo wa Despacito
- Kisela yaikimbiza wasikudanganye na Eneka ya Daimond
Naye Charlie Puth alionesha kufurahishwa zaidi na hatua aliyofikia ya kushiriki katika wimbo huo, akikumbuka miaka kumi iliyopita ambapo video ya kwanza ya wimbo wake rasmi ulipata kuangaliwa mara 10,000 tu kwenye YouTube.
“Ninakumbuka niliposaini mkataba na YouTube mwaka 2007 na nikaweka video yangu ambayo ilifikisha watazamaji 10,000. Leo ni muongo mmoja umetimia, ninajisikia furaha kuu kuwa sehemu ya video ambayo imeangaliwa mara nyingi zaidi YouTube,’ Puth anakaririwa.
Wimbo huo ulioachiwa mwaka 2015 na kutumika kama ‘sound track’ kwenye Fast and Furious 7, umebeba ujumbe mzito wa majonzi kwa ajili ya kumbukumbu ya marehemu Paul Walker.