Vyombo vya usalama nchini Somalia vinawashikilia walimu saba wa shule binafsi nchini humo kwa tuhuma za kufanya vikao vya siri na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

Kwa mujibu wa taarifa za kukamatwa kwa walimu hao, wanatuhumiwa kupanga njama ya kuanza kufundisha kwa kutumia mtaala utakaokuwa unasaidia kufundisha itikadi za kundi hilo la kigaidi.

Kila mwalimu anadaiwa kuwa na shule yenye watoto takribani 1,000 ambao wana umri kati ya miaka saba na 15, ambao wako kwenye hatari ya kufunzwa itikadi kali za kidini zinazoendana na matakwa ya kundi hilo.

Kwa mujibu wa waziri wa habari wa Somalia, Mahad Hassan Osman, walimu hao walibainika na kukamatwa katika mji wa Jowhar.

“Walikuwa wanajaribu kubadili mtaala wa shule kuendana na imani ya kundi hilo, ambayo ni utekelezaji wa sera na itikadi kali za kutumia sharia,” BBC inamkariri waziri huyo.

Alifafanua kuwa walimu hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili baada ya upelelezi kukamilika.

Al-Shabaab wanaendesha vita dhidi Serikali ya Somalia kwa takribani miaka 10 na sasa wako katika ushirika na kundi hatari la kigaidi la Al-Qaeda.

Mbunge Chadema awaomba wananchi waliombee taifa
Wiz Khalifa avunja rekodi ya YouTube na wimbo aliomuimbia Paul Walker