Wizara ya Afya, imekusudia kutoa chanjo kwa watoto zaidi 2000 ambao hawakupata chanjo kwa sababu mbalimbali na watoto 1700 ambao hawakumalizia chanjo, huku wito ukitolewa kwa jamii kutoa ushirikiano katika zoezi hilo, ili kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya Magonjwa yanayozuilika.

Akizindua rasmi Mfumo wa uraghibishaji wa Huduma za Chanjo Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo amesema mfumo huo utasaidia kupata huduma kwa urahisi huku akiwapongeza Wataalam kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Ofisi ya Rais TAMISEMI, pamoja na Jiji la Dar Es Salaam kwa kuja na Programu hiyo.

Amesema, “kama unajua kuna maadui maradhi, sehemu kubwa ni kutengeneza mbinu, mimi niwapongeze sana Wataalam kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma , pamoja na wengine kwa kuja na mfumo huu wa uraghibishaji sisi mmetupa daraja la kusimamia hivyo timu zote tusimamie vyema katika kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo katika kumkinga dhidi ya magonjwa.”

Afisa Program ya Uratibu na Elimu ya Afya Maeneo ya Kazi kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Simon Zilimbili, amesema chanjo hiyo itaendeshwa kwa siku 10 katika tarafa mbili(Ukonga na Segerea) kati ya tatu za Wilaya ya Ilala ambapo kupitia mpango huo utasaidia kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo.

Kwa Upande wake Mratibu wa Chanjo Halmashauri Jiji la Dar Es Salaam Martine Kalongolela amesema lengo la zoezi hilo ni kufikia asilimia 100 huku akitoa hofu wananchi na zoezi na hali hiyo itasaidia kumkinga mtoto huku akitolea mfano madhara ya mtoto akikosa chanjo ya Polio ni kusababisha ulemavu au kifo.

Dkt. Kikwete amuwakilisha Rais Samia Mazishi ya Ahtisaari
NEMC, ZEMA kusajili mfuko kuhimili mabadiliko Tabianchi