Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaelekeza Maafisa Masuuli waimarishe usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2023/2024 na kuzitaka Wizara na Taasisi za Serikali zifanye vikao kwa njai ya mtandao, ili kupunguza matumizi.
Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo wakati akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma na kusema vikao kwa njia ya mtandao bila kuathiri tija vitapunguza matumizi makubwa ya fedha za umma za uendeshaji wa vikao vya Serikali.
Amesema, “Watendaji wa Serikali, imarisheni ukusanyaji wa mapato na kufanya matumizi kwa kuzingatia maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2023/2024 sambamba na kubuni vyanzo vipya vya mapato.”
Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa Serikali wazingatie kanuni, sheria na taratibu katika manunuzi na matumizi ya fedha za umma, ili kufikia shabaha na malengo ya uchumi.