Nchini Namibia, Wizara ya afya inasema imethibitisha visa 54 vya homa ya nguruwe kati ya visa 190 vinavyoshukiwa ambapo Wizara ya mambo ya nje ilisema eneo la kati la Otjozundjopa na lile linalozunguka mji mkuu Windhoek ndilo lililoathiriwa zaidi, kwa kuwa na kesi 24 chanya zilizoripotiwa katika kila eneo.
Taarifa za Wizara hiyo ya Afya imesema, kesi hizo, ziliripotiwa kuanzia Julai 2022 hadi sasa (Oktoba 2022), kutoka mkoa wa Otjozondjupa (24 kati ya kesi 37 zinazoshukiwa), Khomas (24 kati ya kesi 138 zinazoshukiwa), na Kavango Mashariki (6 kati ya kesi 15 zinazoshukiwa), ambapo pia vipimo vilihusisha ugonjwa wa Uviko-19 lakini hakukuwa na maambukizi.
Homa ya mafua ya H1N1, pia inajulikana kama mafua ya nguruwe, ni maambukizo ya virusi ya kupumua kwa papo hapo kwa wanadamu, ambayo mara nyingi huonyeshwa na homa, maumivu ya kichwa, myalgia na dalili zingine kama za mafua, na nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, ilikumbwa na mlipuko mkubwa wa homa ya nguruwe mwaka 2009-10.
Wizara ya Afya inasema, wakati zaidi ya visa 8,000 vinavyoshukiwa vikiripotiwa wakati wa mlipuko huo, watu 102 walipimwa na mtu mmoja alikufa, huku Watoto, Wazee na Wanawake wajawazito wakichukuliwa kuwa kundi la watu walio katika hatari zaidi kwa kuweza kupata maambukizi.