Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza rasmi kutumia mfumo wa kielektroniki wa Government electronic Payment Gateway (GePG) katika makusanyo ya kodi ya pango la ardhi pamoja na tozo nyingine zinazotokana na sekta ya ardhi nchini.
Mfumo huo utamrahisishia mwananchi kulipa kodi ya pango la ardhi popote alipo, ikiwa ni pamoja na kulipia tozo nyingine mbalimbali za sekta ya ardhi, pia, kujua anadaiwa kiasi gani cha kodi ya pango la ardhi na kulipia popote alipo bila kusumbuka kufuata huduma hizo katika vituo vya makusanyo.
Aidha, kwa mwananchi yeyote anayemiliki kiwanja au shamba lililopimwa na kuwa na hati, ataweza kutumia simu yake ya mkononi kujua kiasi cha kodi ya pango la ardhi anachodaiwa na kukulipa kwa kutumia simu yake ya mkononi pia.
Vile vile, kwa huduma nyingine za sekta ya ardhi ambazo zinahusisha malipo kama vile upekuzi katika daftari la msajili (official serach), mwananchi atapaswa kutembelea ofisi za Wizara ya ardhi zilizo katika eneo lake na kupatiwa makadirio ya kulipia huduma husika pamoja na namba ya malipo itakayomuwezesha kulipia aidha kwa njia ya benki au simu ya mkononi.
Hata hivyo Wizara hiyo imeandaa mpango maalum wa kutoa mafunzo juu ya matumizi ya mfumo huo kwa kuelemisha mikoa mingine baada ya kupata mafanikio mazuri katika mkoa wa Dar es Salaam. Lengo kubwa la kutumia mfumo huu ni kuongeza ufanisi katilka ukusanyaji wa maduhuli ya serikali pamoja na kurahisisha ulipaji kodi ya pango la ardhi nchini,