Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imetoa ufafanuzi juu ya watahiniwa waliofutiwa matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2022 kuwa, kati ya watahiniwa 560,335 waliofanya mtihani, 337 ndio waliofutiwa matokeo na wengine 20 matokeo yao yamezuiliwa hadi uchunguzi utakapomilika.
Ufafanuzi huo umetolewa hii leo jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ambaye ameongeza kuwa, kati ya waliofutiwa matokeo wanne waliandika lugha isiyo na staha, 51 walikutwa na maandishi yasiyoruhusiwa ndani ya chumba cha mtihani, 10 walikamatwa na simu na smart watch, 9 walifanyiwa mtihani na watu wengine na 27 wakisaidiana katika chumba cha mtihani.
Amesema, “Wengine sita kutoka kituo cha Mnemonic, Zanzibar waligundulika kutumia jukwaa la WhatsApp kupata majibu kutokana na yule mmoja aliekutwa na simu, 206 walikuwa na mfanano wa majibu usio wa kawaida ukihusisha kituo cha mtihani cha Thaqaafa, Mwanza.
Kituo kingine ni Twibhoki cha Mkoani Mara, huku 24 wa kituo cha Cornellius ambacho pia kilikuwa na watahiniwa kutoka shule ya Andrew Father Memorial waligundulika kupewa majibu kabla ya kuingia chumba cha mtihani.”
Waziri Mkenda ameongeza kuwa, Serikali inafanya jitihada kumaliza kabisa tatizo la udanganyifu na
kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watumishi wa umma wote watakaobainika kuhusika na
udanganyifu huo na kwamba kufanya udanganyifu ni sawa na uhujumu uchumi.