Kundi la Wahandisi 40 kutoka kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), wametembelea daraja la Kigongo-Busisi linalounganisha mikoa ya Mwanza na Geita kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu sayansi, teknolojia na uvumbuzi unaotumika duniani kwenye sekta ya ujenzi.

Wakiwa eneo hilo, Mhandisi kundi la Makampuni ya Ushauri wa mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi, Abdukarim Majuto amewaambia Wahandisi wa GGML kuwa mradi huo umejengwa kwa teknolojia ya hali ya juu, inayotumiwa na wahandisi duniani kote.

Alisema, “teknolojia inayotumika katika ujenzi wa miradi mikubwa chini ya maji ni moja ya kivutio cha kutembelea eneo la Daraja la Kigongo Busisi na Daraja lina urefu wa kilometa 3.2 katika Ghuba ya Mwanza na kuunganisha Kigongo mkoani Mwanza na Busisi mkoani Geita, ni moja ya maeneo ya kuvutia zaidi nchini.”

Meneja wa Miundombinu wa GGML, Eliakim Kagimbo, alisema Kampuni inatumia daraja hilo kama jukwaa la kujifunzia ili kupata maarifa ya kina juu ya vipengele vya kiufundi vya mradi mzima na kwamba GGML imetekeleza miradi kadhaa ya uhandisi kwa miaka mingi na daraja hilo linatoa fursa kuboresha ujuzi wao.

Kwa upande wake, Msimamizi wa ujenzi wa TANROAD katika daraja hilo, Mhandisi William Sanga alikaribisha ziara hiyo ya mafunzo na kubainisha kuwa kukamilika kwa daraja hilo ni suala muhimu katika utekelezaji wa programu ya maendeleo ya nchi.

“Daraja la Kigongo–Busisi litakuwa kiungo muhimu kati ya Mwanza na mikoa ya jirani pamoja na nchi jirani. Kwa hivyo lina uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi katika eneo hilo. Daraja hili litapunguza kiasi kikubwa cha foleni katika njia hii na pia kuboresha usalama wa watumiaji katika kivuko cha ziwa hili,” alisema.

Tangu kuanzishwa kwake, GGML imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na mamlaka za serikali za mitaa kusaidia miradi kadhaa ya jamii katika mkoa wa Geita, kupitia ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi pamoja na programu za kitaifa.

Ziara hiyo, ambayo ni sehemu ya mipango ya Kampuni ya GGML kuendeleza wafanyakazi wake kupitia ziara mbalimbali za kimafunzo kwenye miradi mikubwa ya kihandisi, imefanyika mwishoni mwa wiki na ilihudhuriwa na vikundi vya mafundi wakiwemo wahandisi wa mitambo, umeme na viwanda, wasimamizi wa miradi, mafundi mekanika na wakuchomelea vyuma.

Wizara yatoa ufafanuzi waliofutiwa matokeo
Fainali za Kombe la Dunia kurudi zilikoanzia