Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe amewataka wananchi kuwa wavumilivu wakati Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) likifanya jitihada za kufanya uchunguzi katika mfumo mzima wa Gridi ya Taifa na kurekebisha hitilafu iliyopelekea kukosekana kwa umeme katika mikoa yote iliyounganishwa na Gridi ya Taifa.
Profesa Mdoe ameyasema hayo mapema hii leo katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema kuwa tukio la kukatika kwa umeme katika mikoa yote iliyounganishwa na Gridi ya Taifa asubuhi linashughulikiwa huku baadhi ya mikoa ikiwa tayari imeshaanza kupata umeme.
Aidha, amesema kuwa mara baada ya wataalam kutoka Tanesco kugundua hitilafu katika marekebisho hayo, wataalam walianza kushughulikia tatizo hilo na kufanikisha kurejesha umeme katika mikoa yote iliyounganishwa na Gridi ya Taifa.
Ameongeza kuwa uwashaji wa mitambo unaendelea na uchunguzi wa kubaini chanzo cha hitilafu bado unaendelea.
Hata hivyo, Mkurugenzi Msaidizi katika Masuala ya Usafirishaji Umeme Mhandisi Kahitwa Bishaija amesema kuwa mpaka sasa tatizo limeshadhibitiwa.