Kocha Mkuu wa FC Barcelona, Xavi Hernandez amesema ameshangazwa na adhabu ya beki wa Real Madrid, Nacho Fernandez, kupunguzwa na hivyo kumfanya awe huru kucheza mechi ya Clásiço mwishoni mwa juma hili.

Nacho alitolewa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea rafu Portu wa Girona Septemba 30, mwaka huu na awali alifungiwa kucheza mechi tatu.

Hata hivyo, adhabu hiyo ilipunguzwa hadi mechi mbili baada ya kukata rufani juma lililopita, ikimaanisha Nacho, ambaye tayari ametumikia mechi moja ya marufuku hiyo, alikosa mchezo wa juzi Jumamosi (Oktoba 21) dhidi ya Sevilla kabla ya kurejea kumenyana na FC Barcelona Oktoba 28, mwaka huu.

“Ni mshangao kamili,” alisema Xavi katika mkutano na waandishi wa habari alipoulizwa maoni yake juu ya uamuzi huo.

“Msimu uliopita, marufuku ya mechi tatu kwa (Robert) Lewandowski kwa kugusa pua yake haikupunguzwa, kwa hiyo ilikuwa mshangao mkubwa kuona habari za Nacho kupunguziwa hadi mechi mbili.”

Kabla ya kuwakaribisha Madrid kwenye Uwanja wa Olimpiki, Barca wana mechi ya nyumbani dhidi ya Shakhtar Donetsk kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hapo keshokutwa Jumatano (Oktoba 25).

Guardiola: Messi, Haaland wanastahili Ballon d'Or
Tumieni fursa za uwekezaji, toeni ushirikiano - Majaliwa