Na: Josefly
Wingu zito la majonzi limetanda kwenye nyuso za Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla. Taarifa za kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad zimetikisa ardhi ya Taifa la Tanzania, lililoundwa kwa kuchanganya udongo wa pande mbili, Zanzibar na Tanganyika. Tukapata Tanzania.
Maalim Seif ni mmoja kati ya majemedari wa kisiasa, waliowahi kulitumikia Taifa hili kwa z aidi ya miongo mitanohadi alipofikwa na umauti akiwa na umri wa miaka 77.
Tuyapitie angalau kwa muhtasari maisha ya Maalim Seif, mwanasiasa aliyeamua kutumia busara zaidi ya tamaa, akafikiria kuhusu kuwaunganisha watu badala ya kuchochea kuni kwenye malumbano.
Maalim alizaliwa Oktoba 22, 1943, Pemba enzi za utawala wa Sultani wa Zanzibar. Alisoma shule ya msingi Uondwe na Shule ya Wavulana ya Wete zote ziko Pemba. Alimaliza elimu ya kidato cha nne mwaka 1961 na baadaye akahitimu elimu ya kidato cha sita mwaka 1963, zote katika Shule ya Kumbukumbu ya Mfalme George wa VI iliyoko Ngome Kongwe, Zanzibar.
Hata hivyo, kutokana na umahiri wake na kiwango cha juu cha uelewa, Maalim alizuiwa kuendelea na masomo ya Chuo Kikuu kwakuwa alitakiwa kufanya kazi za Serikali kuziba pengo la uhaba wa watumishi wa umma mwaka 1964, baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyokuwa imeingia madarakani kuwaondoa katika mfumo wafanyakazi wengi wa uingereza. Alifanya kazi hiyo kwa kipindi cha miaka tisa (1964-1972).
Maalim alichapa kazi ya ualimu, akawanoa wazanzibari wenzake kielimu, hadi mwaka 1972 alipojiunga na elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hapo, alisomea masomo ya Sayansi ya Siasa, Uongozi wa Umma na Uhusiano wa Kimataifa.
Nafasi alizowahi kushika serikalini:
Mwaka 1977-1980, alikuwa Mjumbe wa Baraza la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Waziri wa Elimu. Mwaka 1980-1989, alikuwa mwakilishi Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Mwaka 1977 alikuwa mwakilishi kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maalim alipata nafasi ya kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia mwaka 1977-1987). Alichaguliwa pia kuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango ya chama hicho tawala kuanzia mwaka 1982 -1987).
Maalim, alichapa kazi kwa uzalendo, hali iliyosababisha aendelee kupanda. Februari 6, 1984 aliteuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, nafasi aliyoitumikia hadi Januari 22, 1988. Baada ya kuondolewa CCM kufuatia mgogoro ndani ya chama hicho, safari yake ya siasa ilipumzika kwa muda kwakuwa kulikuwa na chama kimoja pekee.
Maalim alikutana pia na magumu, kwani maisha ni safari, kuna kupanda na kushuka. Ilifika wakati wa kupanda mlima, ambapo Mei 1989 alifungwa jela hadi Novemba, 1991.
Baada ya Tanzania kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Maalim Seif na wanasiasa wengine walianzisha Chama Cha Wananchi Cuf (CUF). Na safari yake kama kiongozi katika upande wa vyama vya upinzani ikaanza. Maalim akawa Katibu Mkuu wa chama hicho cha upinzani.
Mwaka 1995, aliteuliwa na chama chake kugombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hakufanikiwa kuibuka mshindi katika uchaguzi uliokuwa wa ushindani mkubwa. Alipata asilimia 49.76 ya kura zote. Salmin Amour wa CCM, alishinda kwa kupata asilimia 50.24 ya kura zote.
Mwaka 2000, aligombea tena urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa tiketi ya CUF. Pia, hakufanikiwa, alipata asilimia 32.96 ya kura zote. Amani Abeid Karume wa CCM alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 67.04.
Mwaka wa 2001, CCM na CUF waliafikiana kumaliza mgogoro wa kisiasa kati yao na kuwaunganisha Wazanzibari kwa kusaini makubaliano maalum, maarufu kama MUAFAKA.
Mwaka 2005, alitupa karata yake tena katika kinyang’anyiro dhidi ya Rais Amani Abeid Karume. Hakufanikiwa tena, akipata asilimia 46.07 ya kura zote. Karume alishinda kwa kupata asilimia 53.18.
Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010, Maalim Seif bado alikuwa na nguvu na alishiriki tena kuwania urais kwa tiketi ya CUF. CCM walimsimamisha Dkt. Ali Mohammed Shein. Matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010, Maalim Seif hakufanikiwa tena, baada ya Dkt. Shein kutangazwa mshindi. Uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkubwa zaidi. Maalim alipata kura 175,338, Dkt. Shein alishinda akipata kura 179,809, yaani Maalim alipata asilimia 49.1 na Dkt. Shein asilimia 50.1. Wakaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Maalim akawa Makamu wa Kwanza wa Rais. Uamuzi huo ulitokana na mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar iliyotoa nafasi kwa mshindi wa pili wa urais kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Maalim aliendelea kuwa na moyo wa mwanasiasa aliyekomaa. Hakukata tamaa, aliingia tena kwenye mapambano ya kisiasa huku akiendelea kuhamasisha amani na utulivu. Kwa sababu, kwenye ushindani lazima mmoja ashinde na sio lazima ushinde wewe, aliamini katika kutokata tamaa.
Ilipofika Oktoba 2015, Maalim aliingia tena kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa urais akichuana na Dkt. Ali Mohamed Shein wa CCM. Matokeo ya Uchaguzi huo yalifutwa kabla ya kutangazwa na Tume ya Uchaguzi, baada ya kuelezwa kuwa taratibu hazikufuatwa, hususan uamuzi wa Maalim Seif kujitangaza kuwa ndiye mshindi.
Baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza uchaguzi wa marudio Machi 2016, Maalim alikataa kufanya kampeni kwenye uchaguzi huo, na hata baada ya matokeo chama chake kiliamua kutoshiriki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Wimbi zito la kisiasa lilikipiga Chama Cha Wananchi (CUF) kuanzia mwaka 2017. Kukawa na timu mbili kwenye chama hicho. Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba na Maalim Seif aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama, walitofautiana. Chanzo kikiwa madhara ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, baada ya umoja wa vyama vya upinzani maarufu kama UKAWA kushindwa uchaguzi. Mwenyekiti aliamua kujiuzulu nafasi yake kabla ya uchaguzi, akarejea baadaye akiihitaji nafasi yake ambayo wakati huo ilikuwa wazi. Hilo likawa chanzo cha mgogoro.
Baada ya mchakato mrefu ndani ya chama mahakamani, Machi 2019, Maalim Seif alitangaza kuachana na CUF na kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo. Alitumia msemo uliopata umaarufu, “tunashusha tanga, tunapandisha tanga, safari inaendelea.”
Mwaka 2020, aliwania tena urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa wakati huu ilikuwa kwa tiketi ya ACT Wazalendo. Kwa mara nyingine hakufanikiwa.
Kwa busara na tafakuri ya muda, Maalim alikubali kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Desemba 8, 2020 Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwingi alimuapisha kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Leo, Februari 17, 2021 amepumzika kwa amani, baada ya kuvuka milima na mabonde. Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani.