Meneja wa FC Barcelona Xavier Hernández Creus anaamini Mshambuliaji Kinda wa klabu hiyo Lamine Yamal Nasraoui Ebana atakuwa na mafanikio makubwa siku za usoni baada ya kucheza kwa mara ya kwanza katika kikosi cha kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania, ‘La Liga’ dhidi ya Real Betis juzi Jumamosi (Aprili 29).
Yamal alitambulishwa kama mbadala wa dakika za lala salama pale Camp Nou wakati Barca ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Betis, na kurejesha uongozi wao wa alama 11 kileleni.
Nyota huyo ambaye ni zao la Kituo cha Kukuza na kuendeleza vijana cha La Masia, mwenye umri wa miaka 15 na siku 290, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya LaLiga kuichezea FC Barcelona.
Yamal nusura atengeneze bao la dakika za lala salama na Ousmane Dembele, lakini winga huyo akayumba mbele ya lango, na Xavi anaamini kuwa kiungo huyo ana kipaji cha kufanya vema hapo mbeleni.
Kocha huyo wa Barca amesema: “Nimemwambia ajaribu mambo. Akiwa na umri wa miaka 15, ni kipaji na mchezaji maalum.
“Anaweza kufunga, amesaidia na ukimuona kwenye mazoezi unaona anaweza kuwa mkubwa sana.” Raphinha alifunga bao moja na kusaidia jingine katika kipigo cha Betis, huku Andreas Christensen na Robert Lewandowski pia wakifunga na Guido Rodriguez alijifunga.
Winga huyo wa Brazil aliunga mkono maoni ya Xavi kuhusu Yamal, akisema: “Nilipokuwa na umri wa miaka 15, niliichezea timu ya jirani yangu. “Inashangaza. Ingekuwa ajabu kufunga bao.”
Raphinha alipendekeza Barca lazima warudie uchezaji wao kama vile ule dhidi ya Betis, ambao ulikuwa tofauti kabisa na mchezo wao wa Jumatano katika kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Rayo Vallecano.