Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete amewataka viongozi wa Klabu ya Yanga kurudisha hamasa ya ushabiki wa mpira katika klabu hiyo.
Ameyasema hayo katika harambee ya kuichangia Yanga iliyojulikana kama ‘KUBWA KULIKO’ iliyofanyika jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali na Taasisi binafsi.
Amesema kuwa kwasasa mashabiki wa timu ya Yanga hawana hamasa ya kuishangilia timu yao, hivyo amewataka viongozi wa timu hiyo kutatua changamoto zinazo wakabiri.
”Mimi huwa siendi mpirani, lakini naangalia kwenye TV, mashabiki wa Simba ni moto kweli kweli, lakini upande wa Yanga ni bariiiidi, mnatatizo gani nyie?mna nini? hapana viongozi mnatakiwa mlibadirishe hili,”amesema Rais Mstaafu JK
Aidha, amewataka viongozi kubadirisha hali hiyo kwani kipindi cha nyuma klabu hiyo haikuwa imepooza kiasi cha kupoteza morali kwa mashabiki wake.
Hata hivyo, Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete amewataka mashabiki na wapenzi wa klabu ya Yanga kuungana kwa pamoja ili kutatua changamoto zinazoikabiri timu hiyo.