Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya kutengeneza na kusambaza mbolea ya Yara Tanzania, Winstone Odhiambo amesema wamejipanga kuhakikisha wanatua changamoto zilizojitokeza katika msimu wa wa Kilimo uliopita, kitu ambacho kitasaidia ufikiaji wa malengo na ukuzaji wa Kilimo nchini.
Odhiambo ameyasema hayo wakati wa mjumuiko na Wasambazaji wa Mbolea ili kupanga mikakati ya ya msimu na kuhakikisha mbolea inapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu kipindi hiki ambacho msimu wa kilimo umekaribia.
Amesema, “Tunashukuru Serikali ya awamu ya sita imejipanga na hata msimu uliopita tulipata ruzuku ambayo ilisaidia kwa kiasi kikubwa na kwa mwaka huu tunatarajia kufikia malengo na kuhakikisha changamoto za msimu uliopita hazijitokezi na pia tuyafikie malengo ili kilimo kilete tija.”
Kwa upande wake mmoja wa Wasambazaji wa Pembejeo za Kilimo katika Mikoa ya Njombe na Ruvuma, Deogratius Mtewele amesema ushirikiano wao na Yara umesaidia kuleta ufanisi katika sekta ya Kilimo, huku Hawa Muhina toka Kata ya Kahe Kilimanjaro akisema mpango huo utawasaidia wao kama mawakala na Wakulima wanaotumia Mbolea za Yara.