Raia wa Marekani, Michael Job ambaye amejizolea umaarufu nchini Kenya akijulikana kama ‘Fake Jesus’ (Yesu bandia) ameonekana tena mitaani siku chache baada ya kudaiwa kuwa amefariki dunia.
Job amekuwa gumzo hususan katika nchi za Afrika Mashariki kupitia mitandao ya kijamii kutokana na kufanana na muigizaji wa Hollywood aliyekuwa mhusika mkuu wa filamu ya maisha ya Yesu.
Tangu alipoingia nchini Kenya, amekuwa akihusishwa na mambo mengi huku taarifa mbalimbali za uongo zikiwa zinatengenezwa kuhusu yeye. Hivi karibuni, taarifa ya kufariki kwake ilisambaa na kuandikwa na vyombo vingi vya habari ikiwa ni pamoja na vyombo vikubwa nchini Kenya na Tanzania.
Hata hivyo, BBC imeeleza kuwa Job ambaye ni mhubiri wa injili nchini humo jana alionekana akifanya ziara zake za kuhubiri, Nakuru.
Mhubiri huyo pia jana aliweka ujumbe kwenye mtandao wa Facebook akieleza kuwa huduma yao ya kuhubiri injili imepokelewa vizuri na kwamba mamia ya watu wamempokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao.
“Leo, mimi na Paul Maurer tumepata fursa ya kuhubiri. Mamia ya mioyo ya watu wamefanya uamuzi wa kumkubali Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Watoto wengi wanampokea Yesu, Bwana asifiwe,” ameandika kwenye akaunti yake ya Facebook.
“Nenda ulimwenguni kote na uhubiri injili kwa kila kiumbe. Nenda nje na uhubiri injili kwa mtu mmoja leo. Mungu atakujazi, anakusubiri wewe. Ubarikiwe, asante kwa kutuombea!” Aliongeza.