Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans kimeondoka jijini Dar es salaam kuelekea nchini Algeria tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza wa Kundui D, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Young Africans itaanza kuwania nafasi ya kutinga Robo Fainali ya Michuano hiyo mwishoni mwa juma hili kwa kucheza dhidi ya Mabingwa wa Soka nchini Algeria Chabab Riadhi de Belouizdad ‘CR Belouizdad’.
Kikosi cha Wananchi kimeanza safari mapema leo Jumanne (Novemba 21) Alfajiri kikiwa na baadhi ya wachezaji ambao hawakuitwa katika timu zao za taifa katika kipindi hiki cha michezo ya kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’.
Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema wanakwenda Algeria kwa ajili ya kupambana na wana uhakika wa kuzinyakua alama tatu muhimu kutoka kwa wapinzani wao, kutokana na uzoefu mkubwa walionao kwa sasa, baada ya kufanya makubwa msimu uliopita wakishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho.
Kamwe amewataka Mashabiki na Wanachama wa Young Africans kuiombea timu yao wakati wote wa safari na itakapokuwa katika mchezo huo muhimu, ili kufanikisha malengo yanayowapeleka nchini Algeria.
“Tunaondoka na baadhi ya wachezaji ambao tulikuwa nao kambini katika kipindi hiki, wengine ambao wapo na timu zao za taifa wataungana nasi nchini Algeria,”
“Lengo kubwa linalotupeleka nchini Algeria ni kushindana na wapinzani wetu na tuna matumaini tutafanikiwa kuondoka ugenini tukiwa na alama tatu muhimu mikononi mwetu, tunafahamu mchezo hautakuwa rahisi, lakini wachezaji wetu wameandaliwa kupambana”
“Tuna uzoefu wa kutosha wa kupambana katika michezo ya ugenini, msimu uliopita tulifanya hivyo na tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa wakati tukishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho, itikadi ya kupambana katika viwanja vya ugenini itaendelea maradufu msimu huu In Shaa Allah.”
“Tunachowaomba Mashabiki na Wanachama wa Young Africans waiombee timu yao katika kipindi chote cha safari na tutakapokuwa katika mchezo wetu, lengo ni kupata ushindi.” amesema Ally Kamwe.
Kundi D la Ligi ya Mabingwa Barani Afrika lina timu za Young Africans, Chabab Riadhi de Belouizdad ‘CR Belouizdad’ (Algeria), Al Ahly (Misri) na Medeama SC (Ghana).